Na Jackline Minja, New York, Marekani Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, ameieleza Jumuiya ya Kimataifa hatua kubwa zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kulinda na kuendeleza haki za watu wenye ulemavu, wakati aliposhiriki Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (COSP19) unaofanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Jijini New York, Marekani. Mhe. Mahundi, ambaye amemuwakilisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Palamagamba John Kabudi, amesema Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo ya kisheria, kisera na kiutendaji ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki, fursa na huduma stahiki kama wananchi wengine. Akiwasilisha taarifa ya nchi, Mhe. Mahundi amesema Tanzania imepiga hatua kubwa kupitia Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010 kwa Tanzania Bara pamoja na Sheria Na. 8 ya mwaka 2022 ya Zanz...